Tuesday, December 31, 2019

MIUNDOMBINU YA SHULE IKAMILIKE MAPEMA-MAJALIWA


*Kama kuna wahusika walioko likizo warudishwe haraka

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema miradi yote ya ujenzi wa miundombinu ya shule ikamilike mapema na kama kuna watendaji walioko likizo warudi kwani Serikali inataka wanafunzi wote waanze masomo pamoja.

Ameyasema hayo leo (Jumanne, Desemba 31, 2019) wakati alipofanya ziara kukagua ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleoa wilayani Ruangwa. Amesisitiza ukamilishwaji wa miradi hiyo ili wananchi waanze kuitumia.

Waziri Mkuu amesema agizo alilolitoa kwa wakuu wa mikoa Desemba 29, 2019 kuhusu usimamizi wa miundimbinu ya shule ikiwemo ujenzi wa madarasa liko pale pale kwa sababu Serikali haitaki kuona wanafunzi wakipishana katika kuanza masomo.

Miradi ambayo Waziri Mkuu ameitembelea ni ujenzi wa shule ya msingi ya Ng’au ambayo ipo katika hatua za mwisho kukamilika, ujenzi wa chuo cha VETA, hospitali ya wilaya ya Ruangwa na shule ya sekondari ya Lucas Maria. 

Waziri Mkuu amesema Serikali inatoa fedha kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo hivyo ni lazima viongozi katika maeneo husika wahakikishe wanashirikiana katika kusimamia utekelezaji wake.

Amesema wanafunzi wanatakiwa kuanza masomo mwanzoni mwa mwezi Januari, 2020, hivyo ni lazima usimamizi ukaongezwa katika baadhi ya maeneo ambayo miundombinu yake bado haijakamilika ili kuwahi masomo.

Akiwa katika shule ya Sekondari ya Lucas Maria Waziri Mkuu amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Andrea Chezue ahakikishe mafundi wanafanya kazi usiku na mchana.

“Shule zinakaribia kufunguliwa na baadhi ya majengo kama bwalo, maabara, nyumba za walimu hayajakamilika mafundi hawapo eneo la ujenzi na Serikali imetoa fedha. Nataka kazi hii ikamilike mapema kwani hakuna sababu.”

Wakati huo huo, Wananchi wa Wilaya ya Ruangwa wamepongeza na kumshukuru Rais wa Awamu ya Tano Dkt. John Pombe Magufuli kutokana na miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini.

Wananchi hao wakiwemo vijana wanaojenga chuo cha VETA walitoa pongezi na shukrani hizo mbele ya Waziri Mkuu baada ya kumaliza kukagua mradi wa ujenzi wa chuo hicho. Mafunzo yatakayotolewa chuoni hapo ni pamoja na ufundi uashi, seremala, magari, ushonaji nguo na Tehama.

Kadhalika, vijana hao wamewashauri vijana wenzao wajitokeze na kuchangamkia fursa za ajira zinazopatikana katika maeneo yao kupitia miradi mbalimbali inayotokelezwa na Serikali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua vitanda katika Shule ya Lucas Maria, iliyopo wilayani Ruangwa, wakati akikagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua darasa katika Shule ya Msingi Ng’ao, iliyopo wilayani Ruangwa, wakati akikagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akiuliza jambo kwa Mshauri wa Mradi Sudi Shomari, wakati alipotembelea mradi majengo ya VETA, yanayojengwa katika Kata ya Nandagala wilayani Ruangwa, wakati akikagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua mradi wa majengo ya VETA, yanayojengwa katika Kata ya Nandagala wilayani Ruangwa, wakati alipotembelea miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua maabara ya hospitali mpya ya Wilaya ya Ruangwa, wakati alipokagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua maabara ya hospitali mpya ya Wilaya ya Ruangwa, wakati alipokagua miradi ya Halmashauri, Desemba 31, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akifafanuliwa jambo, baada ya kukagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa ofisi za Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa, wakati alipokagua miradi ya Halmashauri hiyo, Desemba 31, 2019.

Read More

Sunday, December 29, 2019

WAZIRI MKUU ATOA AGIZO KWA WAKUU WA MIKOA

*Ataka ujenzi wa vyumba vya madarasa ukamilishwe

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza wakuu wa mikoa nchini wahakikishe wanasimamia ipasavyo ujenzi wa vyumba vya madarasa vikamilike kwa wakati ili wanafunzi wote waliochagulia kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2020 waanze masomo kwa pamoja.

Amesema lengo la Serikali ni kuhakikisha wanafunzi wote wanaanza kusoma kwa pamoja kwa sababu wakipishana muda wa kuanza masomo baadhi yao wanashindwa kufanya vizuri jambo ambalo si sahihi.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumapili, Desemba 29, 2019) wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020 kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM wilaya ya Ruangwa.

Jumla ya watahiniwa  933,369  sawa  na  asilimia  98.55 ya  waliosajiliwa  walifanya  mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2019 na kati yao watahiniwa  759,737  wamefaulu ambao ni sawa na asilimia 81.50.

Kati  yao  wasichana  ni  395,738  ambao  ni  sawa  na  asilimia  80.87  na wavulana  ni  363,999  sawa  na  asilimia  82.20.  Mwaka  2018  watahiniwa waliofaulu  walikuwa  asilimia  77.72,  hivyo  kuna  ongezeko  la  ufaulu  kwa asilimia  3.78. 

“Wakuu wa Mikoa hakikisheni vyumba vya madarasa vinakamilika ili wanafunzi wote waliofaulu waanze masomo kwa pamoja. Kitendo cha wanafunzi kupishana kuanza masomo kinawafanya waliochelewa kutofanya vizuri katika mitihani yao.”

Kadhalika, Waziri Mkuu amewasisitiza viongozi hao wahakikishe wanasimamia vizuri elimu kwa watoto wa kike na kuwachukulia hatua watu wote watakaobainika kuwakatisha masomo iwe kwa kuwaoa, kuwaozoesha au kuwapa ujauzito.

Amesema Serikaliimeweka sheria kali ya kumlinda mtoto wa kike lengo ni kumuwezesha amalize masomo yake ili aweze kujikwamua kiuchumi na aondokane na utegemezi, hivyo ni marufuku kuwakatisha masomo.

“Watoto wa kike wanatakiwa kuheshimiwa katika jamii na Serikali itatoa adhabu kali ya kifungo cha miaka 30 jela kwa mtu atakayekatisha elimu ya mtoto wa kike iwe kwa kumuoa au kumpa ujauzito.”

Waziri Mkuu amesema Serikali inataka kuona idadi kubwa ya watoto wa kike wanatimiza malengo yao kielimu, hivyo ni lazima wakaondolewa vishawishi  kwa kuboresha mazingira yao ya kujifunzia ikiwa ni pamoja na kuongeza idadi ya mabweni.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu ameishukuru Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli kwa kutoa fedha nyingi kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo nchini ikiwemo na wilaya ya Ruangwa ambayo imepewa sh. bilioni 38 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya kimkakati.

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuupongeza uongozi wa halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa kubuni mradi wa kimkakati wa ujenzi wa ghala la kuhifadhia mazao na pembejeo linalojengwa katika kijiji cha Lipande. Ujenzi huo unaogharimu sh bilioni 5.45.

Ghala hilo ambalo limeanza kutumika lina uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 litaiwezesha halmashauri kujiongezea mapato ya ndani na kusaidia kupunguza utegemezi kutoka Serikali Kuu na wafadhili. Pia litapunguza gharama za usafirishaji wa korosho walizokuwa wanatozwa wakulima wakati wa kusafirisha mazao. 

Amesema katika kipindi cha miaka minne ya Serikali ya Awamu ya Tano miradi mingi ya kimkakati imetekelezwa nchini ambayo ni pamoja na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), upanuzi wa bandari za Mtwara, Dar es Salaam na Tanga, uboreshwaji wa viwanja vya ndege, ununuzi wa rada na ununuzi wa ndege mpya.

Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano tangu ilipoingia madarakani mwaka 2015, kipaumbele chake kilikuwa ni kukuza kiwango cha uchumi kutoka cha chini kwenda cha kati ifikapo mwaka 2025 kupitia sekta ya viwanda.

Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ruangwa, wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020, Desemba 29, 2019.
 
Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ruangwa, wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020, Desemba 29, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ruangwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020, Desemba 29, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akizungumza na Wajumbe wa Mkutano wa Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Ruangwa, wakati akitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya 2015/2020, Desemba 29, 2019.



Read More