Monday, October 26, 2020

UCHAGUZI UMEKARIBIA, MJIHADHARI NA WANAOHUBIRI UDINI - MAJALIWA


 

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema uchaguzi mkuu umekaribia sana na amewaonya wana-Lindi na Watanzania wote wajihadhari na viongozi wanaohubiri udini.

 

Ametoa onyo hilo jana (Jumapili, Oktoba 25, 2020) wakati akizungumza kwa nayakati tofauti na wakazi wa kata tano za Kibutuka, Ngunichile, Lionja, Ruponda na Chiola alipokuwa njiani akirejea Ruangwa kutoka Liwale kupitia Nachingwea.

 

Alikuwa wilayani Liwale ambako alienda kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Bw. Zuberi Kuchauka na mgombea ubunge wa jimbo la Nachingwea, Dkt. Amandus Chinguile na madiwani wa kata alizopitia.

 

“Uchaguzi mkuu umekaribia, tuwe makini na wanaohubiri udini. Kiongozi anayehubiri udini huyo hafai kuwa kiongozi wa Watanzania. Wako wengine wanaoanza kuigawa nchi kwa ukanda, ukianza kuigawa nchi kwa ukabila, unaua misingi ya Taifa hili.”

 

“Leo tuko wamoja kwa sababu ya amani iliyodumishwa na waasisi wa Taifa hili. Leo makabila tofauti wanaishi pamoja bila kubaguana. Ndiyo umekuwa utamaduni wetu. Hata hapa kuna Wamasai, Wangindo, Wachaga na kadhalika. Tunahitaji tumchague kiongozi atakayetunza amani ya nchi yetu,” alisisitiza.

 

Alisema: “Natambua, wananchi wenzangu mmekuwa na muda wa miezi karibu miwili wa kufanya tathmini na tafakari ya kina ili nani awe kiongozi wa nchi hii, nani awe mwakilishi wa jimbo hili na nani awe mwakilishi wa kata hii kwa maana ya diwani. Nataka niwahakikishieni kwamba kiongozi anayefaa anatoka Chama cha Mapinduzi,” alisema.

 

“Nimeangalia katika wote wanaotaka kupewa Urais, hakuna kiongozi mwenye hizo sifa zaidi ya Dkt. John Pombe Magufuli. Tulimpa miaka mitano ya kuongoza nchi, amefanya mambo makubwa na nyote mmeona ama kusikia yaliyofanyika kupitia vyombo vya habari.”

 

Akifafanua sifa za kiongozi anayetakiwa, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Tunataka tupate kiongozi mahiri, mzalendo, mwadilifu na mwaminifu ambaye ni lazima tujiridhishe kuwa ataweza kuongoza nchi hii yenye watu zaidi ya milioni 60 na makabila tofauti.”

 

“Hatuhitaji kumchagua Rais ambaye sasa hivi anasema akiwa madarakani ataweka rehani madini yetu ili aweze kupata fedha za kuwawezesha wananchi. Sasa hivi nchi inapata mgao wa madini wa sh. bilioni 500 na ndiyo maana tunajenga hospitali, shule na barabara. Zamani tulikuwa tunapata shilingi bilioni 50 tu.”

 

Aliwataka wakazi hao wamchague Dkt. Magufuli ili apambane na wala rushwa na akawaonya wasimchague kiongozi ambaye amezungukwa na mafisadi au wala rushwa. Aliwataka wakazi hao wamchague Dkt. Magufuli kwa kura nyingi za ndiyo ili aweze kuleta maendeleo na kukamilisha yale mazuri aliyoyaanzisha.

 

“Tunataka kiongozi atakayelinda rasilmali za Taifa hili. Na huyo si mwingine bali ni Dkt. Magufuli. Ndugu zangu wa CHADEMA naomba kura zenu, wana ACT naomba kura zenu, CUF naomba kura zenu, na CHAUMA naomba kura zenu. Mchagueni Dkt. Magufuli awe Rais kwa sababu maendeleo hayana chama,” alisema.

 

Akielezea ni kwa nini anawaomba kura wananchi wa vyama vyote bila kujali itikadi zao za kisiasa, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Ni kwa sababu tunatafuta kiongozi wa nchi. Uongozi wa nchi unataka mtu mchapakazi na mwenye nia ya kuleta maendeleo kwa Watanzania, na huyu si mwingine bali ni Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.”

 

Leo Mheshimiwa Majaliwa anaendelea na kampeni kwenye jimbo la Nanyumbu.

 

(mwisho)

   

Read More

BARABARA YA KILWA-NANGURUKURU-LIWALE KUJENGWA KWA LAMI


 

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema sh. bilioni 1.3 zimetolewa ili kuanza kazi ya upembuzi yakinifu wa barabara ya Kilwa-Nangurukuru-Liwale.

 

Ametoa kauli hiyo jana (Jumapili, Oktoba 25, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Likongowele, wilayani Liwale, mkoani Lindi kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Ujenzi wilayani humo. Pia alizungumza na wakazi wa kata za Kibutuka, Ngunichile, Lionja, Ruponda na Chiola kwa nyakati tofauti alipokuwa akirejea Ruangwa kutoka Liwale kupitia Nachingwea.

 

Alisema barabara ya Kilwa-Nangurukuru-Liwale yenye urefu wa km. 258 upembuzi wake unatarajiwa kuanza wakati barabara ya Liwale - Nachingwea - Ruangwa yenye urefu wa km.185 usanifu wake wa kina unaendelea na ukikamilika zitatafutwe fedha za kuzijenga kiwango cha lami. “Barabara hizi zinapatikana uk. 75 wa Ilani ya CCM ya 2020-2025.”

 

Akifafanua zaidi kuhusu barabara za mji wa Liwale, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. bilioni 1.7 zimetolewa na Serikali kwa ajili ya ujenzi wa barabara za Liwale huku sh. milioni 891 zikitolewa kwa ajili ya matengenezo ya muda maalum na kwa kiwango cha lami kwa barabara za Sanabu – Mangota - Mponda, Mchanda - Ngosha Bucha, Wamao- Soko la Zain na Reiner Club- Nyanga.

 

Akielezea maboresho yaliyofanyika kwenye sekta ya afya, Mheshimiwa Majaliwa alisema sh. milioni 500 zimetolewa kwa ujenzi wa hospitali ya wilaya ya Liwale ambapo ujenzi wa jengo la OPD lipo hatua ya linta na ujenzi wa jengo la maabara lipo hatua ya kuezeka.

 

Alisema kwa mwaka 2020/2021 Halmashauri imepangiwa sh. bilioni moja kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa hospitali hiyo. Kwa upande wa vituo vya afya, alisema sh. bilioni moja zimetolewa kwa ajili ya ujenzi Kituo cha Afya cha Mpengere ambacho kimekamilika na huduma zinatolewa kwa wananchi. “Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kibutuka nao umekamilika na wananchi wanahudumiwa,” alisema.

 

Alisema sh. milioni 69.4 zimetumika kwa ukamilishaji wa zahanati za Mkundi, Chigugu na Barikiwa pamoja na kuchangia ujenzi wa jengo la mama na mtoto. “Pia shilingi bilioni 1.43 zilitolewa kwa ajili ya ununuzi wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi. Fedha za ununuzi wa dawa ni wastani wa shilingi milioni 22.6 kwa mwezi,” alisema 

 

Mheshimiwa Majaliwa alikuwa wilayani Liwale ambako alienda kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Bw. Zuberi Kuchauka na mgombea ubunge wa jimbo la Nachingwea, Dkt. Amandus Chinguile na madiwani wa kata alizopitia.

 

Akiwafafanulia mambo yaliyofanywa na Serikali ikiwa ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ndani ya miaka mitano wilayani humoMheshimiwa Majaliwa alisema kwenye sekta ya maji, sh. bilioni 2.9 zimetolewa kwa ajili ya miradi mikubwa ya maji ikiwemo mradi wa Kipule – sh. milioni 559.2, ambao alisema umekamilika na unatoa huduma maeneo ya Kipule na Mkonganaje.

 

Aliitaja miradi mingine kuwa ni mradi wa maji Likombola ambao umegharimu sh. milioni 355.1 na kwa sasa umekamilika na unatoa huduma maeneo ya Likombola na Kitamamuhi. Mwingine ni mradi wa Maji Mangirikiti uliotumia sh. milioni 135.5 na sasa umekamilika na unatoa huduma vijiji vya Mangirikiti na Kimbamba.

 

Aliitaja miradi mingine ambayo bado inaendelea kujengwa na fedha zake kwenye mabano kuwa ni mradi wa maji Kibutuka (sh. milioni 213.1) ambao unakamilishwa kwa ajili ya Kijiji cha Kibutuka na mradi wa maji Kitogoro (sh. milioni 214) ambao unakamilishwa kwa ajili ya kijiji cha Kitogoro.

 

Mradi wa Maji Mikunya uliogharimu sh. milioni 359 unakamilishwa kwa ajili ya vijiji vya Mikunya na Legezamwendo wakati mradi wa maji Mpigamiti uliojengwa kwa sh. milioni 11 unakamilishwa kwa ajili ya vijiji vya Mpigamiti, Namakororo na Mitawa.

 

Akielezea mpango wa elimu bila ada, Mheshimiwa Majaliwa alisema kwa shule za msingi  55 zilipatiwa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya ukarabati, utawala, michezo, mitihani na posho kwa maofisa elimu kata na walimu wakuu.

 

“Kwa shule za sekondari, shule 16 zilipatiwa kiasi cha shilingi bilioni 1.7 kwa ajili ya fidia ya ada, chakula kwa shule za bweni na posho ya madaraka kwa wakuu wa shule.

 

Leo Mheshimiwa Majaliwa anaendelea na kampeni kwenye jimbo la Nanyumbu.

 

(mwisho)


Read More

Sunday, October 25, 2020

MAJALIWA AHUTUBIA MKUTANO WA KAMPENI LIWALE MKOANI LINDI

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa  akizungumza na mgombea ubunge wa CCM wa Jimbo la Liwale, Zuberi Kuchauka katika mkutano wa kampeni aliouhutubia kwenye  uwanja wa Ujenzi Liwale mkoa wa Lindi, Oktoba 25, 2020
 Mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika Jimbo la Liwale , Zuberi Kuchauka  (wa pili kulia) akicheza muziki wa Sengeli wakati Msanii Shalo Mwamba (kulia) alipoimba katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa kwenye  uwanja wa Ujenzi Liwale mkoa wa Lindi Oktoba 25, 2020.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Ujenzi Liwale mkoa wa Lindi Oktoba 25, 2020.
Wananchi wa Liwale wakimsikiliza Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Ujenzi Liwale mkoa wa Lindi, Oktoba 25, 2020.


Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akihutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Ujenzi Liwale mkoa wa Lindi Oktoba 25, 2020.
 

Read More

MAJALIWA: SERIKALI HAINUNUI KOROSHO, INASADIA UPATIKANAJI WA MASOKO


 

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema Serikali hainunui korosho wala mazao mengine bali inaweka mazingira mazuri ya upatikanaji wa masoko.

 

“Serikali hainunui korosho, Serikali hainunui pamba, wala hainunui chai au kahawa. Kazi ya Serikali ni kutengeneza fursa ili wanunuzi waje. Mtu asitumie zao la korosho ili kujipatia umaarufu wa kisiasa,” amesema.

 

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Oktoba 25, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Likongowele na Kibutuka wilayani Liwale ambako alienda kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Bw. Zuberi Kuchauka na madiwani 20 wa kata za jimbo hilo.

 

“Mwaka 2018, kuna wafanyabiashara waliungana na wakagomea kununua korosho kwa sh. 1,800. Rais Dkt. Magufuli akasema hakuna kununua korosho za wakulima kwa bei hiyo, ndipo akatoa sh. bilioni 900 ili zitumike kununua korosho kwa bei isiyopungua sh. 3,000 kwa kilo.”

 

“Fedha hizo zimetumika kuwalipa wakulima, wasafirishaji, wenye magunia, kulipia usimamizi wa maghala na sasa imebakia kuwalipa Halmashauri ambao wanadai ushuru wa asilimia 5, na hao ni Serikali wenzetu kwa hiyo watalipwa tu. Kama kuna wakulima waliobakia ni mmoja mmoja sana, hao wanafuatiliwa na Wizara husika.”

 

Amesema korosho siyo zao pekee lililoathiriwa na kuporomoka kwa bei bali mazao mengine kama pamba, chai, kahawa na tumbaku nayo yameathiriwa na kushuka kwa bei mwaka huu.

 

“Korosho ni miongoni mwa mazao ya kimkakati nchini yaliyokosa soko msimu uliopita baada ya mataifa ya Ulaya kufunga mipaka yao kutokana na ugonjwa wa corona na hivyo wanunuzi hawawezi kuja nchini.”

 

“Korosho, pamba, tumbaku, chai na kahawa hayakuwa na bei nzuri kutokana na corona si vinginevyo. Serikali hainunui mazao, kazi yake ni kutengeneza mazingira mazuri ya soko asije mtu akawadanganya na kutumia bei za mazao ili apande chati kisiasa,” alionya.

 

Akitoa mfano, Mheshimiwa Majaliwa amesema: “Bei ya pamba imeshuka kutoka sh. 1, 200 hadi sh. 800 kwa kilo; kahawa imeshuka kutoka sh. 1,800 has sh. 1,200 kwa kilo, na tumbaku imeshuka kutoka sh. 1,700 hadi sh. 1,400.”

 

“Wanunuzi wakubwa wa korosho wanatoka China, Singapore, Vietnam na India. Hawa wenzetu sasa hivi bado wameelemewa na ugonjwa huu, hawawezi kutoka na kusafiri. Tuwaombee nchi zao ziondokane na corona ili na sisi tuweze kufanya biashara na nchi nyingine,” alisisitiza.

 

(mwisho)

   

Read More

MAJALIWA: RAIS MAGUFULI AMENITUMA NIJE KUMWOMBEA KURA


 

MJUMBE wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Kassim Majaliwa amesema mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli amemtuma aje amuombee kura kwenye mikoa ya Kusini na amesema hatowaangusha.

 

“Mheshimiwa Rais amenituma nije kumuombea kura kwa sababu wakati anapanga kuja huku kama ilivyokuwa kwenye ratiba ya Tume ya Uchaguzi, akapata ugeni wa kitaifa kutoka kwa Rais wa Malawi, Mheshimiwa Dkt. Lazarus Chakwera.”

 

“Malawi ni jirani zetu, asingeweza kuwaacha. Tume ikishakupangia ratiba na ikapita na wewe hukwenda, haisogezwi mbele bali wanaangalia kama huko mbele utakuwa na nafasi wanakupangia tena,” amesema.

 

Ametoa kauli hiyo leo (Jumapili, Oktoba 25, 2020) wakati akizungumza na wakazi wa kata za Likongowele, wilayani Liwale, mkoani Lindi kwenye mkutano uliofanyika kwenye uwanja wa Ujenzi wilayani humo.

 

Mheshimiwa Majaliwa ambaye yuko Lindi kumuombea kura mgombea urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. John Pombe Magufuli, alitumia fursa hiyo kuwanadi mgombea ubunge wa jimbo la Liwale, Bw. Zuberi Kuchauka na madiwani 20 wa kata za jimbo hilo.

 

Amewaomba wakazi hao wamchague Dkt. Magufuli kwa sababu urais unataka mtu makini atakayejali mahitaji ya watu wanyonge na mwenye mawazo ya kuleta maendeleo kwa wananchi wake.

 

“Lazima tumpate Rais anayeguswa na mahitaji ya wanyonge, anayeweza kusimamia huduma za jamii ili ziwafikie wananchi wote, na mtu huyo si mwingine bali ni Dkt. Magufuli. Jumatano ya keshokutwa, nenda kapige kura kwa Dkt. Magufuli, hata kama unatoka upinzani, kampigie Dkt. Magufuli ili atuletee maendeleo,” amesisitiza.

 

Katika hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka wakazi wa Liwale na wa mkoa mzima wa Lindi wamshukuru Rais Magufuli kwa mambo mazuri aliyowafanyia. “Lazima tumshukuru kwa yote aliyotufanyia kwenye mkoa wetu na Watanzania kwa ujumla kwa kumpa kura nyingi za kishindo,” amesisitiza.

 

“Ni lazima tumshukuru kwa kuniteua niwe msaidizi wake wa karibu. Kwani kuna mikoa mingapi hadi auchague mkoa huu? Kuna Waheshimiwa Wabunge zaidi ya 200 ndani ya Bunge, lakini aliomuona mtoto wenu anafaa na ndipo akamchagua awe msaidizi wake wa karibu,” amesema.

 

(mwisho)

Read More

Saturday, October 24, 2020

MAJALIWA AHUTUBIA MKUTANO WA KAMPENI LIWALE

Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akivua kofia yake ya CCM ili amvishe Msanii Babby Madaha  katika mkutano wa kampeni aliouhutubia kwenye uwanja wa Ujenzi Liwale, Oktoba 25, 2020.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa akimvisha kofia ya CCM Msanii, Baby Madaha katika mkutano wa kampeni aliouhutubia kwenye uwanja wa Ujenzi Liwale, Oktoba 25, 2020.
Mjumbe wa Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu ya Taifa ya CCM, Kassim Majaliwa  akizungumza na Bw. Jivunie Mponda baada ya kuhutubia mkutano wa kampeni kwenye uwanja wa Ujenzi Liwale, Oktoba 25, 2020.
 

Read More

Monday, September 28, 2020

MAJALIWA AHUTUBIA MKUTANO WA KAMPENI - WILAYANI KYERWA

   Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwasalimia wananchi wa Kata ya Kayanga, wilayani Karagwe, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya Changarawe Kayanga, Septemba 29, 2020. 
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwahutubia wananchi wa Kata ya Kayanga, wilayani Karagwe, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya Changarawe Kayanga, Septemba 29, 2020.
Wananchi wa Kata ya Kayanga, wilayani Karagwe, wakimshangilia Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, wakati akiwahutubia, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya Isingiro, wilayani Kyerwa. Septemba 29, 2020.
Mjumbe wa Kamati Kuu, Kassim Majaliwa, akiwakabidhi nakala ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya 2020-2025 Mgombea Ubunge wa Jimbo la Karagwe, Innocent Bashungwa, katika mkutano wa kampeni, uliyofanyika katika viwanja vya Isingiro, wilayani Kyerwa. Septemba 29, 2020. Katikati ni Diwani wa Kata ya Kayanga, Germanus Byabusha.
 

Read More

Monday, September 7, 2020

MAJALIWA: SERIKALI INA FEDHA ZA KUTOSHA


MJUMBE wa Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Taifa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Pombe Magufuli ina fedha za kutosha kwa ajili ya kuwatumikia Watanzania katika kuboresha huduma za jamii zikiwemo za afya, maji, elimu.

 

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Septemba 7, 2020) alipohutubia mkutano wa kampeni uliofanyika katika uwanja wa soko la Holili wilaya ya Rombo mkoani Kilimanjaro wakati akimuombea kura Rais Dkt. Magufuli na mgombea ubunge wa Jimbo la Rombo Profesa Adolf Mkenda na wagombea udiwani kupitia CCM.

 

Mheshimiwa Majaliwa amewataka wananchi wasifanye mzaha siku ya kupiga kura itakapofika, wasimchague mtu kwa sababu ya ushabiki na badala yake wamchague Rais Dkt. Magufuli na wagombea wote wa CCM ili waweze kushirikiana nao katika kuendeleza miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao.

 

“Tunaomba kura zenu wanaHolili na Watanzania wote kwa Rais Dkt. Magufuli ili akaendelee kuboreshe maendeleo katika sekta ya elimu itakayotuwezesha kuwa na wataalamu wengi. Nawaomba mumchague Dkt. Magufuli kwa sababu ameitendea haki nchi yetu na ni kiongozi mcha Mungu na mpenda maendeleo.”

 

Akizungumzia kuhusu changamoto ya upatikanaji wa huduma ya maji safi na salama inayowakabili wakazi wa Holili, Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari Serikali imetoa sh. bilioni 1.5 kwa ajili ya kufanya utafiti wa kina kuona namna watakavyoyatoa maji kutoka Ziwa Chala na kuyasambaza kwa wananchi.

 

Amesema mradi mwingine wa maji unaotekelezwa katika wilaya hiyo ni mradi wa maji Njoro II (Tarakea). “Serikali imekamilisha mradi huu kwa shilingi milioni 200 na unatoa huduma ya maji katika eneo la Tarakea. Malengo ya Serikali kwa sasa ni kutafuta fedha ili kuupanua mradi huo na kuweza kutoa maji katika maeneo mengine ya Tarafa nzima ya Tarekea”

 

Mheshimiwa Majaliwa amesema mradi wa kijiji cha Ngareni wenye thamani ya shilingi milioni 812.4 uliohusisha ujenzi wa tanki la kuhifadhi maji la lita 75,000 na ujenzi wa vituo 15 vya kuchota maji pamoja na ufungaji wa bomba za njia kuu na njia za kusambaza maji umekamilika.

 

Amesema kuwa katika kuhakikisha huduma ya maji na salama inawafikia wakazi wote wa wilaya ya Rombo kikamilifu, Serikali mwezi Julai mwaka huu imevunja Kampuni ya Maji ya Kill Water na kuanzisha Mamlaka ya Maji (ROWASA)

 

  

Read More

MAJALIWA AHUTUBIA MKUTANO WA KAMPENI HOLILI

 

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  Mbunge wa Rombo  na Waziri Mstaafu, Basil Mramba (katikati) na Mkuu wa Mkoa Mstaafu, Isdory Shirima  baada ya kuhutubia mkutano wa kampeni  kwenye uwanja wa soko la Holili wilayani Rombo Septemba 7, 2020.

Naibu Waziri  na Mkuu wa Mkoa mstaafu, Aggrey Mwanri akimnadi Mgombea ubunge wa CCM wa jimbo la Rombo, Profesa Adolf Mkenda  katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwenye uwanja wa Soko la Holili wilayani Rombo, Septemba 7, 2020.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiteta na Mgombea ubunge wa CCM wa jimbo la Rombo, Profesa Adolf Mkenda katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Waziri Mkuu kwenye uwanja wa Soko la Holili wilayani Rombo, Septemba 7, 2020.

Mbunge wa zamani wa Rombo na Waziri Mstaafu,  Basil Mramba (kulia) akimnadi mgombea ubunge wa  CCM jimbo la Rombo, Profesa Adolf Mkenda katika mkutano wa kampeni uliohutubiwa na Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  kwenye uwanja wa Soko la Holili wilayani Rombo Septemba 7, 2020.

Read More

Wednesday, July 15, 2020

MAJALIWA ACHUKUA FOMU ZA KUWANIA TENA UBUNGE WA RUANGWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  na Mkewe Mary Majaliwa wakikaribishwa na Katibu wa CCM wa Wilaya  ya Ruangwa, Barnabas Essau (kulia) wakati walipowasili kwenye Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo kuchukua fomu za kuwania tena Ubunge wa Jimbo la Ruangwa, Julai 15, 2020. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikabidhiwa  fomu za kuwania tena ubunge wa jimbo la Ruangwa na Katibu wa CCM wa wilaya  ya Ruangwa, Barnabas Essau kwenye Ofisi ya CCM ya wilaya hiyo, Julai 15, 2020. Kushoto ni mkewe Mary Majaliwa.


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akionyesha fomu za kuwania tena Ubunge wa Jimbo la Ruangwa baada ya kuzichukua, kuzijaza na kuzirejesha, Julai 15, 2020. Kushoto ni Mkewe Mary Majaliwa. 

Mkuu, Kassim Majaliwa akitia saini kitabu baada ya kurejesha fomu za kuwania tena Ubunge wa Jimbo la Ruangwa, Julai 15, 2020. Kulia ni Katibu wa CCM wa wilaya ya Ruangwa, Barnabas Essau. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akirejesha fomu za kugombea tena ubunge wa Jimbo la Ruangwa kwenye ofisi ya CCM ya wilaya ya Ruangwa baada ya kuzichukua na kuzijaza,kushoto ni Mkewe Mary Majaliwa, Julai 15, 2020.

Read More