Sunday, October 27, 2019

MAJALIWA ASHIRIKI MKUTANO WA NCHI ZISIZOFUNGAMANA NA UPANDE WOWOTE NCHINI AZERBAIJAN

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akishiriki katika Mkutano wa Nchi zisizofungamana na uapande wowote kwenye Kituo cha Mikutano cha Baku nchini, Azerbaijan alikomwakilisha Rais Dkt. John Bombe Magufuli, Oktoba 26, 2019. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri Mkuu, wa Azerbaijan, Ali Ahmedov (kulia) kwenye Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu huyo iliyopo Baku nchini humo, Oktoba 27, 2019. Kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini Urusi ambaye pia ni Balozi wa Azerbaijan, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mimwi.(Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Naibu Waziri Mkuu, wa Azerbaijan, Ali Ahmedov (kulia) kwenye Ofisi ya Naibu Waziri Mkuu huyo iliyopo Baku nchini humo, Oktoba 27, 2019.  (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)


Read More

Saturday, October 26, 2019

TANZANIA YATAKA VIKWAZO DHIDI YA CUBA NA ZIMBABWE VIONDOLEWE

SERIKALI ya Tanzania imelaani vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Serikali ya Marekani dhidi ya Cuba na Zimbabwe kwa sababu vinadhoofisha biashara, uwekezaji na ustawi wa wananchi na imetaka vikwazo hivyo viondolewe.

Tamko hilo limetolewa leo (Jumamosi, Oktoba 26, 2019) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kwenye Mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM) ulioanza leo huko Baku, Azerbaijan.

“Vizuizi na vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa dhidi ya Cuba na Zimbabwe vinadhoofisha maendeleo ya uchumi, uwezo wa kufanya biashara, fursa za uwekezaji na ustawi wa wananchi wake.”

“Tanzania inaungana na Jumuiya ya Kimataifa kutaka yawepo majadiliano ya msingi ambayo yataondoa vizuizi kwa Serikali ya Cuba na vikwazo kwa Serikali ya Zimbabwe ili kuleta mabadiliko ya kiuchumi kwa manufaa ya watu wa nchi hizo,” amesema.

Mwaka 2001, Marekani na Jumuiya ya Ulaya (EU) ziliweka vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Zimbabwe baada ya Serikali ya nchi hiyo chini ya uongozi wa Rais Robert Mugabe kuamua kuchukua ardhi yote iliyokuwa ikimilikiwa na wageni.

Waziri Mkuu ambaye anahudhuria mkutano huo wa Wakuu wa Nchi na Serikali kwa niaba ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli, aligusia mambo kadhaa ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, masuala ya Sahara Magharibi, usalama wa Palestina na msimamo wa Tanzania kwenye Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM).

Kuhusu mabadiliko ya tabia nchi, Waziri Mkuu amesema suala hilo ni mojawapo ya changamoto kubwa zinazoikabili dunia na wanadamu kwa sasa. “Tunaiomba Jumuiya ya Kimataifa iweke njia muafaka ambazo zitasadia kurekebisha tishio ambalo tunakabiliana nalo hivi sasa. Tunazitaka nchi zilizoendelea zitimize ahadi zao na michango ya kifedha, zisaidie kujenga uwezo na kutoa wataalamu watakaozisaidia nchi zinazoendelea,” amesema.



Akizungumzia Sahara Magharibi, Waziri Mkuu amesema suala la kujitawala kwa nchi hiyo limeingia sura mpya baada ya Morocco kujiunga tena na Umoja wa Afrika na kwamba hivi sasa imekuwa mjumbe wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

“Ipo fursa kubwa hivi sasa kwa Umoja wa Mataifa pamoja na mjumbe maalum wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ya kuweza kushirikiana na chombo kipya cha Troika kilichoundwa na Umoja wa Afrika katika kuliangalia suala zima la Sahara Magharibi. Tanzania inaunga mkono jitihada hizo,” amesema Waziri Mkuu.

Kwenye suala la Palestina, Waziri Mkuu amesema Tanzania inatambua kwamba nchi hiyo ina haki ya kufurahia amani na uhuru wake kama ilivyo kwa Israeli, kwa mujibu wa mkataba wa Umoja wa Mataifa. “Ni matumaini yetu kwamba kuendelea kuwepo kwa jitihada za kimataifa, mgogoro huo utapatiwa ufumbuzi katika muda muafaka na mataifa haya mawili yataishi kwa amani na utulivu.”

Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuelezea msimamo wa Tanzania kwenye umoja huo na kusisitiza kwamba Tanzania bado ina imani na chombo hicho. “Tanzania itaendelea kuheshimu kazi zinazofanywa na umoja huu kama ambavyo tumekuwa tukifanya kwa miaka 58 iliyopita. Tunaomba ushirikiano baina ya nchi za Kusini uimarishwe. Ushirikiano baina ya nchi zinazoendelea na zilizoendelea nao pia uimarishwe.”

Amesema: “Serikali ya Tanzania inapongeza uhusiano ulipo baina ya Umoja wa Nchi Zisizofungamana na Upande Wowote (NAM), kundi la nchi 77 (G77) na China na kwamba tunatamani ujizatiti zaidi kutetea maslahi ya umoja huu ambao wanachama wake wengi ni nchi zinazoendelea.”

Waziri Mkuu Majaliwa ameambatana na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro na Balozi wa Tanzania nchini Urusi ambaye pia ni Balozi wa Azerbaijan, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mumwi. 

(mwisho)

IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMAMOSI, OKTOBA 26, 2019.
Attachments area
Read More

Friday, October 11, 2019

WAZIRI MKUU AZINDUA MRADI WA KITALU NYUMBA KWA VIJANA KWA NCHI NZIMA

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano imeamua kupambana na ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuanzisha programu za kuongeza na kurasimisha ujuzi.

“Mwelekeo wa Serikali hivi sasa ni kuendeleza viwanda na viwanda hivi vinahitaji malighafi kutokana na mazao. Tumeamua kuongeza malighafi kupitia kilimo, lengo ni kuwafanya vijana waweze kuajiriwa kwenye sekta hii kubwa ya uzalishaji,” alisema.

Ametoa kauli hiyo jana jioni (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) wakati akizindua mradi wa kitaifa wa mafunzo ya ujenzi na kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalunyumba (greenhouse) kwenye viwanja vya maonesho vya Ngongo, mjini Lindi ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa kwa mwaka 2019.

“Nataka vijana muondokane na dhana ya kwamba kuwa na ajira ni lazima uwe umekaa mezani na umeshika kalamu. Ajira ni kazi yoyote ya halali inayompatia mtu kipato iwe ni biashara ndogondogo, mamalishe au bodaboda.”

Akifafanua kuhusu teknolojia ya kitalunyumba, Waziri Mkuu alisema: “Programu hii inasimamiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu. Serikali inayoongozwa Mheshimiwa Rais Dkt. John Pombe Magufuli imeweka msisitizo kwenye kilimo lakini tunaangalia na aina ya kilimo tulichonacho.”

“Maeneo mengi nchini hayana mvua za kutosha. Kwa hiyo tumeanzisha kilimo cha umwagiliaji kwa njia ya matone na siyo kwa kuchimba mifereji. Kitalunyumba kinahitaji nafasi chini ya robo eka, na humo ndani kuna matuta manne tu. Kwa kutumia tenki la maji, unatumia maji kidogo sana kwa kila mche, kwa sbabu yanatoka kwa matone,” alisema.

Alisema mtu yeyote mwenye eneo la kutosha anaezaa kutumia teknolojia ya kitalunyumba wakiwemo wafanyakazi ili wapate mazao ya kujiongezea mapato. “Unaweza kulima mahindi ukala mwaka mzima, unaweza kulima vitunguu au mboga za majani ukauza na siyo nyanya peke yake, hawa wamepanda nyanya kwa sababu ni mfano tu,” alisisitiza.

Akitaja faida zake, Waziri Mkuu alisema mche wa kwenye kitalunyumba unadumu kwa muda mrefu, haupati magonjwa na unazaa kwa wingi. “Mche mmoja unaweza kuzalisha kilo 30 na ndani ya kitalunyumba kimoja kuna miche 580. Nimeambiwa nyanya tisa tu, zinajaa kilo moja. Hii ni fursa ambayo kila mmoja anaweza kulima akiwa nyumbani kwake,” aliongeza.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, Waziri wa Nchi OWM - Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama alisema Serikali ilifanya utafiti na kubaini kwamba asilimia 56 ya nguvukazi nchini ni vijana lakini wanakabiliwa na changamoto ya kukosa ajira.

“Katika utafiti mwingine wa Serikali, tulibaini kuwa kundi kubwa la vijana linaajiri na kuajiriwa lakini pia vijana hawa wanakosa ujuzi unaotambulika rasmi ndiyo tukaja na mkakati wa Taifa wa uwezeshaji wa vijana kwa kuboresha mazingira na kuwapa stadi na ujuzi mbalimbali unaohitajika katika soko la ajira. Stadi na ujuzi huu utawawezesha kujiajiri na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo.”

Alisema mradi wa kitalunyumba ni mradi wa kiprogramu ndani ya Ofisi ya Waziri Mkuu na umelenga kuwapa vijana stadi za kilimo ili waweze kujiajiri au kuajiri wenzao. “Ofisi yako kupitia programu hii inatekeleza mradi wa kilimo cha kisasa kupitia teknolojia ya kitalu nyumba (greenhose) kwa vijana.”

“Mradi wa kitalunyumba ni ujuzi kwenye shamba wa kuwasaidia vijana kulima mazao ambayo yatawasaidia vijana kupata masoko, yatawasaidia wajiajiri ama kuajiri wenzao na kuongeza pato la Taifa,” alisema.

Alisema uzinduzi uliofanywa katika viwanja vya Ngongo unawakilisha vitalunyumba vyote nchini chini ya mradi utakaohusisha vijana 18,000 ambapo kila Halmashauri ina vijana 100 wanaoshiriki kwenye mradi huo ambao watanufaika na mafunzo ya kilimo cha kisasa.

Alisema hadi Septemba 2019, jumla ya vijana 8,700 kutoka katika Halmashauri 83 za mikoa 12 wamepatiwa mafunzo ya ujenzi na kilimo ndani ya kitalunyumba. Mikoa hiyo ni Mwanza, Iringa, Ruvuma, Shinyanga, Geita, Mbeya, Lindi, Dodoma, Kilimanjaro, Manyara, Kagera na Simiyu. Alisema maandalizi ya kutoa mafunzo kwa vijana kutoka katika Halmashauri 102 zilizobaki za mikoa 14 yamekamilika, na yataanza kutolewa kabla ya Novemba, 2019.

Alisema Ofisi ya Waziri Mkuu imetoa zabuni za kuendesha mafunzo hayo kwa kampuni zinazomilikiwa na vijana wa Kitanzania wenye taaluma za kilimo ambao ni wahitimu wa elimu ya juu kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA). Kampuni zilizopewa kazi ya kufundisha vijana wenzao ni Sokoine University Graduates Corporation (SUGECO), Royal Agriculture Ltd na Holly Green Agriculture  Group Ltd.

(mwisho)
Read More

Thursday, October 10, 2019

WAZIRI MKUU AZINDUA WIKI YA VIJANA KITAIFA LINDI

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewaagiza watendaji katika ngazi zote wahakikishe kuwa vijana wanawezeshwa kushiriki katika shughuli za maendeleo.

Ametoa agizo hilo leo (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) wakati akizindua maadhimisho ya wiki ya vijana kitaifa mwaka 2019 kwenye viwanja vya Mpilipili, nje kidogo ya mji wa Lindi.

“Vijana  tushirikiane na Serikali na kufanya kazi kwa bidii ili kuunga mkono jitihada za Serikali yetu ya awamu ya tano inayoongozwa na Mhe. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuwaletea wananchi maendeleo. Hatua hii itatuwezesha kama Taifa tuvuke na tufikie uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025,” amesema.

Amesema wakati anatembelea mabanda ya maonesho, ameona ubunifu wa kijana ambaye ameunda mashine ya kumsaidia mtoto njiti apate joto na pia amemuona kijana mwingine ambaye amebuni mtambo wa kupukuchua magunia 100 ya mahindi kwa saa.

Pia alitembelea banda la kikundi cha vijana kutoka China, Korea Kusini, Argentina, Arzebhaijan na Tanzania ambao waliishi kwenye mazingira magumu na wakabadilika na wameamua kushiriki maonesho hayo ili kuwabadilisha mtazamo vijana wenzao.

“Nimefurahi kuwaona hawa vijana, ninaamini watashirikiana na wenzao wa hapa kuwabadilisha vijana wa Tanzania ili wawe na fikra endelevu.”

Akizungumzia mikakati ya kuwawezesha vijana kiuchumi, Waziri Mkuu amesema Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Programu ya Kukuza Ujuzi Nchini, imeanza kutoa mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba (greenhouse) katika mikoa yote na Halmashauri zote nchini.

Amesema teknolojia hiyo itawasadia wakulima kupata mazao mengi katika eneo dogo na kupata mazao bora yanayokidhi viwango katika soko la ndani na nje ya nchi. “Kwa kutumia teknolojia hii, vijana wengi watapata ajira katika sekta ya kilimo,” amesema.

Waziri Mkuu amesema mkakati huo ni utekelezaji wa agizo la Chama cha Mapinduzi ambacho kinatambua kuwa sekta ya kilimo ndiyo kimbilio la wananchi walio wengi na kupitia ilani yake ya mwaka 2015 Ibara ya 6 (a) imeielekeza Serikali “kuwawezesha wakulima kupata mafunzo ya kilimo cha kisasa, pembejeo, zana za kisasa na wataalamu wa ugani pamoja na mbinu za kuyafikia masoko ya uhakika ya mazao yao”.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeziagiza Halmashauri zote nchini zitenge maeneo maalum kwa ajili ya shughuli za vijana ikiwa ni pamoja na maeneo kwa ajili ya ujenzi wa viwanda vinavyomilikiwa na vijana.

“Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, hadi mwishoni mwa mwaka jana, zaidi ya ekari 217,882.36 zilikwishatengwa. Ninaziomba Halmashauri zote zisimamie na kutekeleza agizo hilo ili kuhakikisha maeneo hayo yanatumiwa kama ilivyokusudiwa,” amesema.

Moja ya shughuli zitakazofanyika wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Vijana mwaka huu ni kuwa na kongamano la vijana linalojumuisha nchi za Afrika Kusini, Zimbabwe, Msumbiji, Kenya, Uganda na Angola. Miongoni mwa masuala yatakayojadiliwa ni mchango wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius K. Nyerere katika maendeleo ya Afrika; Mabadiliko katika elimu na ukuzaji ujuzi kuelekea uchumi wa kipato cha kati ifikapo 2025; na Matumizi ya sayansi, teknolojia na ubunifu kuelekea uchumi wa viwanda.

Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na wananchi waliohudhuria uzinduzi huo, Waziri wa Nchi OWM - Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama alisema sambamba na maboresho ya Sera ya Elimu na Mafunzo, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeandaa Programu ya kukuza ujuzi nchini ambayo imelenga kutoa mafunzo ya stadi mbalimbali za kazi kwa vijana wa ngazi mbalimbali.

“Mpaka sasa, vijana wapatao 32,736 wameshapata mafunzo na mwaka huu, Ofisi ya Waziri Mkuu vijana wengine 46,000 watapata mafunzo mbalimbali ikiwemo kilimo cha kisasa,” alisema.

Naye, Waziri wa Vijana, Sanaa, Utamaduni na Michezo wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Ally Abeid Karume amewataka vijana kote nchini washikamane kwenye shughuli zao za uzalishaji mali na pia amewasisitizia haja ya kuwa wazalendo.

“Vijana mnategemewa kuwa wazalendo. Kuna tofauti kati ya kuwa raia na kuwa mzalendo. Uraia unaupata kwa kuzaliwa na uzalendo unaonekana kwa vitendo na hasa kwa kuwa na maadili mema,” alisema.

“Pia vijana mnategemewa muendelee kuwa wachapakazi. Naomba msonge mbele zaidi na mfanye kazi kwa bidii ili muweze kumudu ushindani katika mataifa ambayo yako mbele kiteknolojia zaidi yetu. Serikali zenu zote mbili zitaendelea kuunga mkono shughuli za vijana za uzalishaji wa bidhaa zenye ubora wa kimataifa.”

(mwisho)
Read More

MWENGE WA UHURU WAMALIZA MBIO RUANGWA

*Wapitisha miradi yote mitatu iliyozinduliwa

MWENGE wa Uhuru uliokuwa unakimbizwa wilayani Ruangwa, mkoani Lindi umemaliza mbio zake na kukabidhiwa wilayani Nachingwea.

Kiongozi wa mbio za mwenge kitaifa, Bw. Mzee Ali Mkongea amesema miradi mitatu ya maendeleo iliyopangwa kuzinduliwa wilayani humo, imeridhiwa na wataalamu wake.

Miradi hiyo ni mabweni mawili kwenye shule ye sekondari ya wasishana ya Hawa Mchopa, mradi wa maji wa Kitandi katika kata ya Likunja na mradi wa barabara ya lami kwenye kata ya Nachingwea, iliyoko Ruangwa mjini.

Akizungumza na wananchi waliojitokeza kupokea mwenge huo leo asubuhi (Alhamisi, Oktoba 10, 2019) kwenye viwanja vya shule ya msingi Chiola, wilayani Nachingwea, Bw. Mkongea amewataka wananchi wa wilaya hiyo wajitokeze kwa wingi kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na pia wajitokeze kupiga kura siku ya uchaguzi huo, Novemba 24, mwaka huu.

Mapema, akizungumza na wakazi waliojitokeza kuupokea mwenge huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema mwenge wa uhuru unakimbizwa maeneo mbalimbali nchini ili kuwahamasisha wananchi washiriki kwenye shughuli za maendeleo.

“Mwenge wa Uhuru unakimbizwa kwenye maeneo yetu mbalimbali ili kuwahamasisha wananchi wajitokeze kushiriki kwenye miradi ya kujiletea maendeleo. Pia unaendana na kumbukumbu ya kifo cha Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na hivyo, tunakumbushwa kuyaenzi mawazo yake,” alisema.

Mbali ya kuwahimiza washiriki kujiandikisha kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Waziri Mkuu alisema kuna makundi manne ambayo yanapaswa kushiriki uboreshaji wa taarifa zao kwenye Daftari la Mpiga Kura pindi zoezi hilo likianza.

“Wanaotakiwa kushiriki zoezi hili, ni wale waliopoteza vitambulisho vyao au wanavyo lakini vimefutika; waliohama maeneo yao na wako kwenye maeneo mapya ambako watapigia kura mwakani; waliokuwa na umri chini ya miaka 18 mwaka 2015 na sasa wamezidi umri huo; na wale ambao mwakani wanatarajia kufikisha umri wa miaka 18,” alisema.


Mapema, akizungumza baada ya kupokea mwenge huo saa 2:45 asubuhi, Mkuu wa Wilaya ya Nachingwea, Bi. Rukia Muwango alisema leo utakimbizwa kwenye wilaya hiyo ambapo miradi yenye thamani ya sh. milioni 781.5 itazinduliwa.

Kesho (Ijumaa, Oktoba 11) mwenge huo utaenda Liwale, Jumamosi (Oktoba 12) utaenda Kilwa na Jumapili (Oktoba 13) utakuwa Manispaa ya Lindi ambako utahitimisha mbio hizo na kuzimwa Oktoba 14, mwaka huu.

(mwisho)
Read More

Wednesday, October 9, 2019

MAJALIWA ASHIRIKI MAPOKEZI YA MWENGE WA UHURU WILAYANI RUANGWA

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru wakati mwenge huo ulipopokelea wilayani Ruangwa katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Nangumbu, Oktoba 9, 2019.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati aliposhiriki Katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Ruangwa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Nangumbu wilayani humo, Oktoba 9, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Mzee Ali Mkongea  wakati mwenge huo ulipopokelewa wilayani Ruangwa katika uwanja wa Shule ya Msingi ya Nangumbu, Oktoba 9, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Mzee Ali Mkongea  wakati alipozungumza katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Ruangwa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Nangumbu wilayani humo, Oktoba 9, 2019. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim, Mgandilwa.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na wakimbiza Mwenge wa Uhuru wakati aliposhiriki katika mapokezi ya Mwenge huo wilayani Ruangwa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Nangumbu wilayani humo, Oktoba 9, 2019. Wa tatu kushoto ni Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru, Mzee Ali Mkongea na wa nne kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa. 

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwa ameubeba Mwenge wa Uhuru wakati aliposhiriki katika mapokezi ya Mwenge huo wilayani Ruangwa yaliyofanyika katika uwanja wa Shule ya Misngi ya Nangumbu, Oktoba 9, 2019. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa na kushoto ni Kiongozi wa Mbio za Mwenge, Mzee Ali Mkongea.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea Mwenge kutoka kwa mmoja wa wakimbiaza Mwenge wa Uhuru, Nkwimba Madirisha Nyangogo wakati aliposhiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Ruangwa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Nangumbu, Oktoba 9, 2019. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Ruangwa, Hashim Mgandilwa.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akipokea Mwenge kutoka kwa mmoja wa wakimbiaza Mwenge wa Uhuru,Nkwimba Madirisha Nyangogo wakati aliposhiriki katika mapokezi ya Mwenge wa Uhuru wilayani Ruangwa yaliyofanyika kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Nangumbu, Oktoba 9, 2019.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akikimbiza Mwenge wa Uhuru wakati ulipopokelewa  kijijini kwake  Nandagala wilayani Ruangwa, Oktoba 9, 2019. Kushoto ni Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru, Mzee Ali Mkongea. 


Read More