Friday, October 26, 2018

SERIKALI YAITAKA WIZARA YA KILIMO IJITATHMINI

*Yaagiza Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Koroshokurudishwa wizarani


RAIS Dkt. John Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini kutokana na suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea pamoja na utendaji wa Bodi ya Korosho Tanzania.

Pia Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Kilimo kumrudisha wizarani Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania (CBT) Prof. Wakuru Magigi baada ya kutoridhishwa na utendaji wake.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Oktoba 26, 2018) katika kikao chake na wakuu wa mkoa ya inayolima korosho kilichofanyika kwenye ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

“Haturidhishwi na utendaji wa bodi ambao amekiuka maelekezo ya msingi ya Serikali katika kusimamia mfumo mzima wa zao la korosho uliopelekea kuvurugika kwa minada.”

Kutokana na hali hiyo Waziri Mkuu amesema Serikali imesitisha minada yote ya korosho nchini kuanzia leo na kuwataka wakulima wawe watulivu wakati ikishughulikia suala hilo.

Kiongozi huyo wa Bodi ya Korosho analalamikiwa kwa kufanya kazi bila ya kushirikisha ushirika wa zao hilo na kutotambua mamlaka zilizowekwa kisheria kama mkuu wa mkoa.

Mbali na malalamiko hayo pia anadaiwa kuendesha operesheni kwa kutumia silaha na askari  dhidi ya viongozi wa ushirika kinyume cha taratibu za nchi. 

Hivyo, Waziri Mkuu amemuagiza Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Lindi na wa  Mtwara wahakikishe gari lenye namba T 814 DDM pamoja na dereva wake linatafutwa popote.

Waziri Mkuu amesema gari hilo ndilo linalodaiwa kutumika katika kuwakamata viongozi wa ushirika waliokuwa wanawasimamia wananchi waliokataa kuuza korosho kwa bei ndogo.

Amesema baada ya dereva wa gari hilo kukamatwa ahojiwe na aeleze askari hao alikuwa anawatoa wapi na nani aliyemtuma. Ameagiza askari wote waliohusika watafutwe.

“Bodi imekuwa ikiwatisha na kuwalazimisha wakulima na viongozi wa ushirika kukubali kuuza korosho kwa bei ya chini jambo ambalo Serikali haiwezi kulikubali.”

Waziri Mkuu amesema Serikali haiwezi kulifumbia macho suala hilo kwa sababu limekuwa likiipaka matope kwani mkurugenzi huyo alikuwa anaingiza askari katika mikoa hiyo bila ya mamlaka kuwa na taarifa.

Kadhalika Waziri Mkuu ameitaka Wizara ya Kilimo kutokaa kimya pindi zinapotokea changamoto kama hizo na badala yake watoe taarifa mapema. “Mambo kama haya yanatokea alafu wizara mmekaa kimya tu.” 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anawapongeza wakulima wa korosho kwa uamuzi wao wa kukataa kuuza kwa bei ndogo na kwamba yuko pamoja nao.

“Rais Dkt. Magufuli ameitaka Wizara ya Kilimo ijitathmini katika suala la mauzo ya zao la korosho linavyoendelea,” amesema Waziri Mkuu.

Pia Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli anataarifa kwamba kuna baadhi ya watendaji Serikalini wanatumia vibaya jina lake kwamba lazima wahusika wote watachukuliwa hatua. 

Awali, Mkuu wa Mkoa wa Mtwara Bw. Gelasius Byakanwa na Mkuu wa mkoa wa Lindi Bw. Godfrey Zambi walilalamikia kitendo cha Prof. Magigi kuvuruga mfumo wa uuzaji wa korosho.

Pia walisema licha ya kumshauri kiongozi huyo juu ya namna bora ya kuendesha minada ya uuzaji wa korosho hakuwasikiliza na kwamba hakuwa tayari kushirikiana nao na pia alikuwa akidharau mamlaka zao. 

Pia alikuwa akiingiza askari na kuwatisha na kukamata viongozi wa ushirika bila ya wao kujua jambo ambalo walisema limezua taharuki kwa watendaji wa ushirika.
Read More

MAJALIWA AKUTANA NA WAKUU WA MIKOA YA LINDI, MTWARA, PWANI NA RUVUMA NA VIONGOZI WA BODI YA KOROSHO KUJADILI BEI YA KOROSHO

Washirki wa Mkutano ulioitishwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  uliowajumuisha Wakuu wa Mikoa  ya Lindi, Mtwara, Ruvuma na Pwani ambao mikoa yao imeanza kuuza korosho, Wenyeviti wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Watendaji Wakuu wa Bodi ya Korosho wakimsikiliza Waziri Mkuu wakati alipozungumza nao kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Oktoba 26, 2018.  
Aliyekuwa  Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Profesa Wakuru Magigi amerejeshwa Wizara ya Kilimo, Oktoba 26, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa  akizungumza  na  Wakuu wa Mikoa  ya Mtwara, Lindi, Pwani na Ruvuma  ambayo inalima  korosho na  imeanza kuuza zao hilo, wakuu  wa wilaya za mikoa hiyo, Wenyeviti  wa Vyama Vikuu vya Ushirika katika mikoa hiyo na Viongozi wa Juu wa Bodi ya Korosho Tanzania  kwenye ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Oktoba 26, 2018. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi na kushoto ni  aliyekuwa Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Korosho Tanzania, Profesa Wakuru Magigi.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na  Wakuu wa Mikoa  ya Lindi, Mtwara, Pwani na Ruvuma  ambao mikoa yao imeanza kuuza korosho, Wenyeviti wa Vyama Vikuu vya Ushirika na Watendaji Wakuu wa Bodi ya Korosho kwenye ukumbi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Oktoba 26, 2018. Kulia ni Naibu Waziri wa Kilimo, Omari Mgumba.


Read More