Tuesday, November 20, 2018

RAIS DKT. MAGUFULI AAHIRISHA MAADHIMISHO YA SHEREHE ZA UHURU


*Aagiza fedha zilizotengwa zikatumike katika kujengea hospitali Dodoma

Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha maadhimisho ya siku ya Uhuru, Disemba 9, 2018 na fedha zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha shamrashamra hizo ameelekeza zitumike kujenga hospitali mkoani Dodoma ambayo itaitwa Uhuru Hospitali.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo (Jumanne, Novemba 20, 2018) na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Rais Dkt. Magufuli ameagiza kiasi cha shilingi milioni 995.182 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe hizo zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali mkoani Dodoma.

Waziri Mkuu ametoa taarifa hiyo wakati alipokutana na viongozi waandamizi wa mkoa wa Lindi pamoja na wilaya zake katika kikao cha maandalizi ya shughuli za kuzima Mwenge kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano kwenye ofisi wa Mkuu wa Mkoa wa Lindi.

Amesema hospitali hiyo itakayojengwa katika eneo la kati ya barabara ya kwenda Hombolo na Chamwino  kwenye barabara ya kwenda Dar es Salaam itakuwa inawahudumia wakazi wa mkoa wa Dodoma pamoja na wananchi wengine watakaokuwa  mkoani humo.

Kadhalika, Waziri Mkuu amesema Rais Dkt. Magufuli amewaagiza wakuu wa mikoa na wilaya waandae matukio watakayoyatekeleza katika maeneo yao yatakayoashiria maadhimisho ya siku ya Uhuru. “Wanaweza kutumia siku hiyo kwa kufanya usafi maeneo ya wazi au kwenye hospitali.”

Kufuatia maagizo hayo, Waziri Mkuu amewataka wananchi katika maeneo yote nchini wajiandae kufanya shughuli mbalimbali za kijamii zitakazopangwa na wakuu wao wa mikoa na wilaya kufanyika katika maeneo yao.


(mwisho)
Read More

WAZIRI MKUU AWAPONGEZA WANANCHI KWA UJENZI WA SHULE

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamewapongeza wakazi wa kata ya Nachingwea wilayani Ruangwa kwa kujenga shule ya msingi  kwenye kijiji cha Kilimahewa.

“Uamuzi wa kujenga shule ya msingi ni sahihi kwa kuwa huwapunguzia watoto kutembea umbali mrefu na pia utarahisisha mazingira ya kusomea kwa watoto wetu.”

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Jumanne, Novemba 20, 2018) alipotembelea eneo la ujenzi wa shule ya msingi Lugalo na kuwataka waendelee na moyo huo.

Amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt. John Magufuli inataka kila mtoto aliyefikia umri wa kwenda shule aanzishwe shule na asome. 

Kadhalika, Waziri Mkuu ametaka wananchi hao waweke pembeni itikadi zao za kisiasa na badala yake washirikiane kujenga miradi ya maendeleo kwenye eneo lao. 

Nae, Mtendaji wa Kijiji cha Kilimahewa, Majuto Ungulu amesema ujenzi wa shule hiyo uliibuliwa na wakazi wa kijiji hicho, ambacho hakina shule ya msingi.

Majuto amesema watoto wa kijiji hicho wanalazimika kutembea umbali wa kilomita mbili hadi shule la msingi Ruangwa, hivyo ujenzi huo utawawezesha kusoma karibu.

Amesema kwa sasa wameanzia na ujenzi wa vyumba vinane vya madarasa, matundu 18 ya vyoo na ofisi mbili za walimu ambapo jumla yake ni sh. milioni 399.8. 

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ametembelea kituo cha afya cha Mbekenyera  na kusema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa na kuwataka wananchi wakitunze.

Amesema kwa sasa wananchi hao hawana sababu ya kulipa nauli kwenda Ruangwa kufuata huduma za vipimo na matibabu katika hospitali ya wilaya.

Ametaja baadhi ya huduma zinazopatikana kwa sasa kwenye kituo cha Afya Mbekenyera ambazo awali hazikuwepo ni upasuaji, maabara, mama na mtoto. 

Mapema, Waziri Mkuu alikagua eneo la ujenzi wa kituo cha Polisi Ruangwa, alitembelea mradi wa ujenzi wa Mahakama ya wilaya na kukagua ujenzi wa ofisi ya mkuu wa Wilaya.

 (mwisho)

Read More

Monday, November 19, 2018

WAZIRI MKUU AWATAKA WANANCHI WAJENGE MABWENI


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwaamewataka wananchi kwenye Kata ya Mnacho wilayani Ruangwa washirikiane kujenga mabweni katika shule ya sekondari Mnacho ili kuwaondolea wanafunzi adha ya kutembelea umbali mrefu kwenda shuleni hapo.

Ameyasema hayo leo (Jumatatu, Novemba 19, 2018) wakati alipotembelea shule hiyo kwa ajili ya kukagua mradi wa ujenzi wa bweni, ambalo ujenzi wake unagharimu sh. milioni 92.4 ikiwa ni mchango uliotolewa na wadau wa elimu.

“Bweni hili likikamilika litawapunguzia wanafunzi kutembea umbali mrefu kuja shuleni hususani wanaoishi vijiji vya mbali kwa sababu wataishi hapa, jambo ambalo litachangia kuongeza ufaulu wa watoto wetu.”

Kadhalika, Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwataka wananchi waishio katika Kata hiyo na za jirani washirikiane na kuanzisha mradi wa ujenzi wa mabweni mengine kwa kuwa hilo moja lililojengwa na wadau halitoshi kulingana na idadi ya wanafunzi.

Amesema yeye yuko tayari kuendelea kuwaunga mkono wananchi hao kwenye mipango yao yote ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika Kata yao, lengo likiwa ni kuhakikisha mikakati ya Serikali ya kuboresha huduma za jamii inatimia.

Hata hivyo, Waziri Mkuu amewataka wananchi hao washirikiane na walimu kufuatilia maendeleo ya taaluma kwa watoto wao shuleni na kujiridhisha kama wanafanya vizuri darasani na iwapo watabaini changamoto waweze kuzitatua kwa pamoja.  

Akisoma taarifa ya ujenzi wa bweni hilo, Mkuu wa shule ya sekondari Mnacho, Mwalimu David Mwakalobo amesemma ujenzi wa bweni hilo lenye uwezo kulaza wanafunzi 80 ulianza Septemba 19, 2018 na unatarajiwa kukamilika Januari, 2019.

“Kutokana na idadi ya wanafunzi waliopo shuleni bweni hili litakidhi mahitaji ya kuwalaza wanafunzi wa kike tu. Tunaendelea kuwaomba wahisani waendelee kutusaidia ili tupate bweni lingine kwa ajili ya kuwalaza wanafunzi wa kiume.”

Mwalimu Mwakalobo amesema iwapo watafanikiwa kuwa na mabweni ya kuwalaza wanafunzi wote 334 shuleni hapo yatawasaidia katika kutatua changamoto ya utoro na mdondoko wa kitaaluma kwa wanafunzi kwa sababu wengi wanatoka mbali.

Pia mradi wa ujenzi wa mabweni utasaidia walimu kuwa karibu na wanafunzi wakati wote, hivyo kupata muda mwingi wa kuwasaidia wanafunzi kimasomo kwa sababu watakuwa wanaishi shuleni. “Mradi huu pia utapunguza wanafunzi wengi wa kike kupata ujauzito.”

Ameongeza kuwa uwepo wa mabweni shuleni hapo utaongeza ari ya wanafunzi kupenda shule tofauti na hali ilivyo sasa kwa sababu wengi wanalazimika kutembea muda mrefu kwa kuwa wanatoka vijiji vya mbali, jambo linalowafanya wasipende shule.


 (mwisho)
Read More

WAZIRI MKUU AZINDUA MSIKITI NA KUSISITIZA UTUMIKE VIZURI


*Awataka waumini wautumie kwa kufanya ibada na kuhamasisha amani
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Msikiti wa Nandagala wilayani Ruangwa, Novemba 19, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi baada ya kuzindua Msikiti wa Nandagala wilayani Ruangwa, Novemba 19, 2018.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wananchi baada ya kuzindua Msikiti wa Nandagala wilayani Ruangwa, Novemba 19, 2018.
 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza wakati alipozindua Msikiti wa Nandagala wilayani Ruangwa, Novemba 19, 2018.


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amezindua msikiti wa Nandagala na amewataka waumini wa dini ya Kiislamu katika Kata ya Nandagala wilayani Ruangwa wautumie vizuri msikiti huo kwa kufanya ibada na kuhamasisha amani na si vinginevyo.

“Msikiti huu ninauzindua leo (jana) naomba tuutunze vizuri na tuutumie kwa kufanya ibada na si ibada za kiuanaharakati. Watakaokuja msikitini na kufanya mambo ya hovyo Mwenyezi Mungu atawalaani.”

Waziri Mkuu alizindua msikiti huo jana jioni (Jumatatu, Novemba 19, 2018), ambapo alitumia fursa hiyo kuwasisitiza waumini wa dini ya Kiislamu kuhakikisha muda wa kufanya swala unapofika waende msikitini hapo kufanya ibada.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliwataka waumini hao waanzishe madrasa na kuwafundisha watoto quran lengo likiwa ni kuwafundisha misingi ya dini na kuwaandaa vizuri na kuwawezesha kukua kiimani ili waje kuwa waja wema.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alimshukuru Mzee Suleiman na familia yake kwa uamuzi wao wa kujitolea kujenga msikiti huo ambao utawawezesha waumini katika kijiji cha Nandagala kufanya ibada zao. “Namshukuru na Mzee Mamboleo na mkewe kwa kutoa eneo lao bure ili litumike kujengea msikiti.”

Kwa upande wake Sheikh Hilal Kipozeo ambaye alihudhuria uzinduzi wa msikiti huo aliwasisitiza waumini wa dini ya Kiislam watumie muda mwingi kwa ajili ya kufanya ibada na wajiepushe na vitendo vyenye kumuasi Mwenyezi Mungu na wadumishe amani.

“Mtume Muhammad (S.A.W) baada ya kutoka katika mji wa Makka na kuhamia Madina kitu cha kwanza alijenga msikiti ili watu waweze kumwabudu Mwenyezi Mungu, alijenga soko ili watu washiriki shughuli za kiuchumi na alifanya upatanishi kwa makabila mawili kwa lengo la kuonesha kuwa kuishi kwa amani ni kitu bora.”

Wananchi na waumini wa dini ya Kiislamu katika kijiji cha Nandagala walimshukuru mfadhili aliyejenga msikiti huo kwa sababu utawawezesha kuwa na eneo la kufanyia ibada baada ya lile la awali kubomolewa kwa kuwa walijenga katika hifadhi ya barabara.

 (mwisho)

Read More

Sunday, November 18, 2018

WAZIRI MKUU AIPONGEZA HALMASHAURI YA WILAYA YA RUANGWA


*Ni baada ya kushika nafasi ya kwanza matokeo ya darasa la saba kwa mkoa wa Lindi

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameipongeza halmashauri ya wilaya ya Ruangwa kwa kushika nafasi ya kwanza katika matokeo ya mtihani wa kumaliza darasa la saba kwa mkoa wa Lindi mwaka huu. 

Amesema Serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Dkt. Magufuli imefanya maboresho makubwa kwa sekta ya eilimu nchini ikiwa ni pamoja na kufuta michango yote ya hovyo iliyokuwa ikiwakera wazazi na walezi.

Waziri Mkuu ametoa pongezi hizo leo (Jumapili, Novemba 18, 2018) katika mkutano wa kuwapongeza walimu wa wilaya ya Ruangwa na baadhi ya wanafunzi waliofanya vizuri katika mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu.Aliongeza kuwa  matokeo ya mwaka jana halmashauri ya wilaya ya Ruangwa ilishika nafasi ya tano kimkoa na kitaifa ilikuwa nafasi ya 141, ambapo kwa mwaka huu imepanda na kuwa nafasi ya kwanza kimkoa na kitaifa kuwa nafasi ya 84. 

Kufuatia matokeo hayo mazuri Waziri Mkuu kwa kushirikiana na halmashauri ya wilaya ya Ruangwa imetoa zawadi mbalimbali kwa kata tatu bora zilizofanya vizuri, shule 10 bora, walimu ambao wanafunzi wao wamepata daraja A katika masomo mbalimbali wanayofundisha pamoja na wanafunzi 10 bora.

Miongoni mwa zawadi hizo ni pamoja na fedha taslimu, kompyuta kwa ajili ya matumizi ya shule zilizofanya vizuri, ikiwa ni kichocheo cha kuongeza  bidii ili mwakani wapate matokeo mazuri zaidi.

Awali, akizungumza katika hadhara hiyo, Mke wa Waziri Mkuu, Mama Mary Majaliwa aliupongeza uongozi wa mkoa wa Lindi kwa mikakati waliyoiweka kwa ajili ya kuboresha elimu, ambayo imesababisha kupatikana kwa matokeo hayo mazuri.

“Nawapongeza kwa sasa mimi kitaaluma ni mwalimu hivyo nafahamu ili mwanafunzi apate matokeo mazuri ni lazima mwalimu afanye juhudi kubwa zitakazomuwezesha mwanafunzi kufaulu masomo yake.”

Alisema matokeo mazuri ya wanafunzi ndiyo yatakayowafanya walimu wafurahi. “Matokeo haya yasiishie hapa mwakani tuongeze bidii tuweze kupata matokeo mazuri zaidi yatakayotuwezesha kushika nafasi ya kwanza Kitaifa.”

Kwa upande wake, Afisa Elimu Msingi wa wilaya ya Ruangwa, Mwalimu Selemani Mrope alisema kuanzia mwaka 2015 hadi 2017 hali ya ufaulu wa wanafunzi wa darasa la saba haikuwa nzuri kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ya utoro.

Mwalimu Mrope alitaja sababu nyingine kuwa ni walimu kutowajibika ipasavyo, ufuatiliaji na usimamizi duni wa taaluma shuleni, ambapo viongozi wengi wa shule na kata walishindwa kusimamia ipasavyo majukumu yao na kuwaacha walimu wafanye kazi kwa mazoea.

“Wazazi wengi kukosa kuwajibika ipasavyo katika elimu ya watoto wao na kuona elimu haina maana kwao na kushindwa kuwahimiza watoto kwenda shule na kusababisha utoro huku wengine wakidiriki kuwashawishi watoto wao wafanye vibaya kwenye mitihani yao.”

Baada ya tathmini waliamua kuweka lengo la ufaulu wa asilimia 80 kwa mwaka huu na asilimia 90 mwaka 2019, hivyo walishirikisha wadau wote wakiwemo viongozi wa Serikali, walimu, wanafunzi, wazazi, viongozi wa dini, wazee maarufu na viogozi wa siasa.



(mwisho)
Read More

MECHI YA YANGA NA NAMUNGO, UWANJA WA MAJALIWA RUANGWA


Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwapungia wapenzi wa mpira wa miguu baada ya kukagua timu za Yanga na Namungo zilizocheza mechi ya kirafiki kwenye uwanja wa Majaliwa katika Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Novemba 18, 2018. Kulia kwake ni mkewe Mary , wapili kushoto ni Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga na kushoto ni Mkuu wa Mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi. Timu hizo zilitoka sare 1-1.
Deus Kaseke wa Yanga akimili mpira katika mechi ya kirafiki kati ya timu yake na Namungo iliyochezwa kwenye uwanja wa Majaliwa katika Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Novemba 18, 2018. Timu hizo zilitoka sare  1 – 1.

Andrew Vincent wa Yanga akizuia mpira kwa kichwa huku akizongwa na  Reliant Lusajo wa Namungo katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa Majaliwa katika Halmashauri ya wilaya ya Rungwa Novemba 18, 2018. Timu hizo zilitoka sare 1 – 1.

 Mshambuliaji wa Yanga, Maka Edward   (kulia) akipiga  mpira huku akizuiwa na  beki wa Namungo, Hashim Manyanya katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa Majaliwa katika Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa, Novemba 18, 2018. Timu hizo zilitoka sare 1-1.

 Kiungo na mshambuliaji wa Yanga, Thaban Kamusoko akijaribu kufunga kwa tikitaka bila mafanikio mbele ya beki wa Namungo FC, Juma Jamal akimkabili katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye uwanja wa Majaliwa katika Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Novemba 18, 2018. Kushoto ni Kipa wa Namungo FC,  Adam Oseja.

Reliant Lusajo wa Namungo FC  (kushoto) akimiliki mpira huku akizongwa na Juma Abdul wa Yanga katika mechi ya kirafiki iliyochezwa kwenye Uwanja wa Majaliwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Novemba 18, 2018. Katika mchezo huo timu hizo zilitoka sare  1-1.

Mashabiki wa Yanga wakishangilia wakati timu yao ilipofunga bao katika mechi ya kirafiki kati ya timu hiyo  na Namungo kwenye uwanja wa Majaliwa katika Halmashauri ya wilaya ya Ruangwa Novemba 18, 2018.  Timu hizo zilitoka sare 1-1.
Read More